Matumaini ya kikosi cha Young Africans kufanya vizuri kwenye mchezo wa mzunguuko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mbeya City FC, yameanza kuonekana, kupitia maandalizi ya timu hiyo yanayoendelea jijini Dar es salaam.
Young Africans walianza msimu wa 2020/21 kwa kuambulia alama moja iliyotokana na sare ya bao moja kwa moja dhidi ya Tanzania Prisons, hali ambayo ilionyesha kutowaridhisha mashabiki na wanachama wa klabu hiyo.
Kocha mkuu wa Young Africans Zlatko Krmpotic, amethibitisha kuanza kuona nuru ya mabadiliko, kufuatia uwezo wa wachezaji wake kwa kudai wanaendelea kuimarika kupitia maandalizi wanayoyafanya.
Amesema kila mchezaji ameanza kuonyesha utayari wa kuelekea pambano dhidi ya Mbeya City FC ambalo litaunguruma uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es salaam mwishoni mwa juma hili.
“Kwa namna ambavyo wachezaji wanacheza kuna kitu cha kipekee ambacho kipo kwao, imani yangu ni kwamba baada ya muda watakuwa tayari kutoa kilicho bora kwa kuwa kwa sasa wanashindwa kwa kuwa bado hawajawa na muunganiko mzuri.”
“Mwanzo wa sare sio mbaya kwani nimeona namna ambavyo wachezaji walikuwa wakicheza kwa kuwa ni mchezo wa kwanza huwezi kulaumu, kinachofuata kwa sasa ni kuendelea kujipanga kwa ajili ya mechi zinazofuata,” amesema.
Kocha Zlatko aliwaambia waandishi wa habari mara baada ya mchezo dhidi ya Tanzania Prisons, wachezaji wake hasa wazawa, walionyesha kutokua na pumzi ya kutosha, jambo ambalo anaamini lilisababisha mpambano huo kushindwa kutoa matokeo chanya kama ilivyokua inatarajiwa.