Serikali kupitia Wizara ya Afya, imesema sababu iliyochangia idadi ya vifo vya Wanawake wanaojifungua kwa njia isiyo ya kawaida ni kupoteza damu nyingi wakati au baada ya upasuaji, damu kuganda na maambukizi ya Bakteria.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel na kusema Wizara ilifanya ufuatiliaji wa vifo kuanzia mwaka 2018 hadi 2021 na kubaini Dawa za ganzi (nusu kaputi), na upasuaji wa kumtoa Mtoto tumboni vilichangia vifo 58 (3.3%) mwaka 2018.
Amesema, “Vifo vingine ni vile vipatavyo 80 (4.8%), kwa mwaka 2019, vifo 65 (4.0%) mwaka 2020, na vifo 65 (4.1%) kwa mwaka 2021.”
Aidha, ameongeza kuwa Wizara kwa ushirikiano na Wataalamu wameanza kuwajengea uwezo Watumishi wa vituo vya Huduma za Afya kuanzia ngazi ya Zahanati hadi Hospitali za Taifa, kwenye eneo la utoaji wa huduma ya nusu kaputi na upasuaji.