Baadhi ya wadau wa mjadala wa kitaifa wa Nishati safi ya kupikia, wameunga mkono wazo la serikali kuja na mpango wa kuachana na matumizi ya mkaa pamoja na kuni na kuhamia katika matumizi ya nishati zingine kama gesi, umeme, jua na bio-gas, ili kulinda afya ya mwanamke ambaye ni muathirika mkuu wa athari za kiafya zitokanazo na kuni na mkaa.

Wakizungumza hii leo Novemba 2, 2022 jijini Dar es Salaam, wadau hao wamesema utumiaji wa nishati safi ya kupikia utaepusha mambo mengi yaliyokuwa yakiwaletea madhara wananchi, ikiwepo athari za kiafya, uharibifu wa mazingira na kupoteza muda mwingi wa kutafuta kuni na kukosa ushiriki wa shughuli za kimaendeleo.

Washiriki wa mjadala, Nishati safi ya kupikia.

Denis Mashauri, ambaye ni mmoja wa washiriki wa mjadala huo amesema, “Huwezi kuelewa madhara ya moja kwa moja ya matumizi ya nishati isiyo safi ya kupikia, lakini ukifika kijijini mama zetu wanateseka wanakohoa na hata wakitumia dawa hawapati nafuu kumbe ni athari za muda mrefu walizoishi nazo, sasa wakati sahihi umefika tubadili huu mfumo.”

Kwa upande wake Injinia Mary Kasamala, amesema ipo mifano mingi ya athari zitokanazo na utumiaji wa kuni ambazo hutoa moshi mwingi wakati wa kupika na kwamba utumiaji wa nishati safi ya kupikia utasaidia kuokoa muda mrefu wa kukaa jikoni na pia kumtua mama mzigo wa kuni kichwani.

Washiriki wakifuatilia mjadala wa kitaifa wa Nishati safi ya kupikia.

“Siwezi kusema kwamba hakuna athari za kuacha kutumia kuni na mkaa maana kuna watu watakosa ajira na hata kipato chao kitapungua lakini hiyo ni bora kwani watu wengi wameathiriwa na utafutaji kuni na wengine wamepoteza ndotonzao kimaisha kwa kubakwa au kuumwa na wadudu wenye sumu wakati wakihangaika kupata hitaji hilo hivyo binafsi naungana na Serikali kuhusu hili tutumie nishati safi ya kupikia.

Mjadala huo wa kitaifa wa nishati safi ya kupikia, umeingia katika siku yake ya pili na ya mwisho, kwa wajumbe kujadili njia mbalimbali za kufanikisha mpango huo uliozinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan Novemba Mosi, 2022.

Azam FC yaivimbia Mtibwa Sugar
Mbunge atoa tahadhari sheria ulinzi taarifa binafsi