Baada ya Azam kukusanya alama tatu mbele ya Ihefu FC juzi Jumatatu (Oktoba 31) katika Uwanja wake wa Azam Complex-Chamazi jijini Da es salaam, Azam FC imeitangazia vita Mtibwa Sugar.

Azam FC itacheza ugenini Manungu Complex mkoani Morogoro juma lijalo, huku ikiwa nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara nyuma ya Simba SC na Young Africans inayoongoza msimamo huo.

Afisa Habari wa Azam FC Hashim Ibwe amesema wameanza kujiandaa kuikabili Mtibwa Sugar ambayo imetoka kujeruhiwa na Simba SC kwa kufungwa mabao 5-0.

Amesema wanatambua mchezo huo utakua mgumu, lakini mikakati waliojiwekea ni kuhakikisha wanakwenda ugenini na kuendeleza wimbi la ushindi kama walivyofanya kwa Ihefu FC na Simba SC.

“Tumeanza kujiandaa kukabilia Mtibwa Sugar, baada ya kumalizana na Ihefu FC, Azam FC imedhamiria kutwaa ubingwa msimu huu hivyo tutapambana bila kuchoka katika viwanja vya ugenini na hapa nyumbani Dar es salaam,”

“Tunafahamu tunakwenda kupambana na timu ya aina gani, ipo katika hali gani na itacheza vipi kwa kile kilichoikuta kwenye mchezo wake wa mwisho, kwa kuzingatia hilo Benchi letu la Ufundi limeanza mikakati ya kusuka mbinu ambazo zitakisaidia kikosi chetu kuendelea kufanya vizuri dhidi ya Mtibwa Sugar.”

“Kikubwa tunawaomba Mashabiki wetu waendelee kuiamini timu yao, kwa sababu upande wa viongozi unafanya kazi usiku na mchana ili kufanikisha mahitaji yote ambayo yatatupa ushindi na kufikia malengo tuliojiwekea msimu huu wa 2022/23.” amesema Ibwe.

Azam FC inakwenda kukutana na Mtibwa Sugar, huku Mshambuliaji wake kutoka Zimbabwe Prince Mpumelelo Dube akiwa katika kiwango cha hali ya juu, baada ya kuifungia mabao muhimu na ya ushindi kwenye michezo dhidi ya Simba SC na Ihefu FC.

Nusu kaputi yachangia vifo wanaojifungua kwa upasuaji
Wadau waunga mkono matumizi Nishati safi ya kupikia