Kaimu Kocha Mkuu wa Simba SC Juma Ramadhan Mgunda amesema mwenendo wa kikosi chake unamfurahisha kutokana na kasi ya wachezaji wake, ambao wakipambana na kupata matokeo mazuri katika Mshike Mshike wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Simba SC inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na alama 17, baada ya kuifunga Mtibwa Sugar mabao 5-0 Jumapili (Oktoba 30), katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Kocha Mgunda amesema kadri siku zinavyozidi kusogea, amekua akiona mabadiliko ya kiwango cha juu kwa wachezaji wake, ambao wana jukumu la kupambana kuipatia matokeo Simba SC.

Amesema ya kikosi chake, yanakuja kutokana na namna anavyokaa na mastaa wake na kuwafundisha namna ya kucheza kama timu ili kufunga zaidi na kuipa timu matokeo chanya.

“Timu nzuri ni ile inayopata matokeo na kucheza vizuri, Simba kwa sasa tunafanya hivyo na tutaendelea kuboresha pale tunapokosea ili kuendelea kuwa bora zaidi.” amesema Mgunda

“Kadri siku zinavyozidi kwenda naona mabadiliko mazuri ndani ya kikosi changu na wachezaji wanaanza kucheza vile ninavyotaka na tunavyowaelekeza mazoezini.”

“Kumalizika kwa mchezo ndio mwanzo wa maandalizi ya mchezo ujao, tunarudi kambini kujipanga kwa ajili ya mchezo wetu dhidi ya Singida Big Stars.

“Tumewaona wakicheza na wana timu nzuri hivyo tukiwa kambini kwetu tutaandaa mbinu na njia sahihi za kupambana nao ugenini na kuhakikisha tunapata ushindi.”amesema Mgunda

Hadi sasa Simba SC ndiyo inaongoza kwa mabao mengi kwenye Ligi Kuu (17) na kuwa timu iliyofungwa machache zaidi (4) huku safu yake ya ushambuliaji ikiwa ndiyo inaongoza kwa kupachika mabao mengi.
Mabao hayo ya Simba SC, 14 yamefungwa na washambuliaji akiongoza Phiri mwenye matano, akifuatiwa na Okrah (3), Sakho (2), Kyombo (2), Chama (1) na Dejan Georgijevic aliyeondoka na bao moja huku mengine mawili yakifungwa na viungo Mzamiru Yassin na Jonas Mkude wenye moja kila mmoja na jingine likiwa ni la kujifunga kwa beki wa Dodoma Jiji, Abdallah Shaibu ‘Ninja’.

Mashabiki Young Africans washushwa PRESHA
TPLB: Hakuna mabadiliko Ligi Kuu