Bodi la Ligi Kuu Tanzania Bara ‘TPLB’ imetangaza kuwa haitafanya mabadiliko kwenye ratiba ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu 2022/23, kama ilivyokua misimu miwili iliyopita.

‘TPLB’ imekua ikifanya hivyo kutokana na changamoto mbalimbali zinazotokana na mazingira ama muingiliano wa ratiba za Michezo ya Kimataifa, lakini safari hii imetoa msimamo huo kupitia kwa Afisa Mtendaji Mkuu Almas Kasongo.

Kasongo amesema Ratiba ya Ligi Kuu msimu huu haitakua na mabadiliko yoyote, na badala yake Michezo itachezwa kama ilivyopangwa, ili kwenda na muda uliokadiriwa hadi kufikia mwisho wa msimu huu.

“Misimu miwili mfululizo tumeshindwa kutekeleza ratiba na mipango, Uviko-19 iliingilia kati tukashindwa kumaliza ligi kwa wakati, hayo hatutaki yatokeee tena msimu huu Ratiba itafuatwa HAKUTAKUWA na mabadiliko yoyote.” amesema Kasongo

Msimamo huo wa TPLB umekuja kufuatia malalamiko yaliyotolewa na Kocha Mkuu wa Young Africans Nasriddin Nabi, kuhusu kikosi chake kukabiliwa na Ratiba ngumu ya michezo ya Ligi Kuu.

Nabi alilalamika mbele ya waandishi wa habari kwa kudai kikosi chake kimekua kikicheza kila baada ya siku tatu ama nne, jambo ambalo ni changamoto kubwa kwa wachezaji wake, kutokana na mazingira ya Michezo ya Kimataifa inayowakabili.

Tayari Mizunguuko 10 ya Ligi Kuu msimu huu 2022/23, imeshachezwa kwa baadhi ya timu za Ligi Kuu, huku timu nyingine zikicheza mizunguuko 9 hadi 8.

Juma Mgunda awapa tano wachezaji Simba SC
Profesa ‘autikisa’ mjadala Nishati safi ya kupikia.