Aliyekuwa Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu amewashukuru Watanzania ambao wamekuwa naye katika maamuzi magumu aliyoyafanya ya kuachana na CCM pamoja na kujiuzulu nafasi yake ya Ubunge kupitia chama hicho.
Amesema kuwa hoja zilizopo mbele kwa sasa ni kubwa kuliko mtu mmoja mmoja na zinalenga kuleta utashi kwa kila Mtanzania kutafakari na kushiriki kikamilifu katika safari ya kuendeleza nchi katika Demokrasia, uchumi na kijamii.
“Nachukua nafasi hii kumshukuru kila mmoja wetu aliyenitumia salaam na kuunga mkono hatua niliyochukua. Hoja zilizo mbele yetu ni kubwa kuliko mtu binafsi na zinalenga kuhuisha utashi wa kila Mtanzania kutafakari na kushiriki kikamilifu safari ya kuiendeleza nchi yetu Kidemokrasia, kiuchumi, na kijamii. Ni maombi yangu kuwa, ujasiri ukaondoe roho ya woga, upendo uondoe chuki, nia njema iondoe kuoneana, na kweli ituweke huru na iondoe roho ya kusingiziana kunakoleta kuumizana na sintofahamu ya hali ya juu,”amesema Nyalandu
Hata hivyo, Nyalandu amekanusha taarifa inayosambazwa ikionyesha kuwa alikuwa ana chat kupitia kundi la Whatsapp na baadhi ya viongozi wa CHADEMA akiomba kujiunga na chama hicho akionyesha kuwa alifanya madhambi wakati akiwa Waziri wa Maliasili na Utalii na kusema kuwa huo ni uzushi wa kutungwa na kusema ni siasa za kizamani hizo