Rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump anatarajia kufika mbele ya Mahakama ya Miami iliyopo jimbo la Florida nchini Marekani hapo kesho Jumanne Juni 13, 2023 ili kusikiliza mashtaka yanayomkabili kuhusiana na nyaraka za siri za serikali zilizokutwa kwenye makazi yake huko Florida.
Trump amefunguliwa mashtaka kutokana na jinsi alivyoshughulikia nyaraka za siri za Serikali, baada ya kuondoka ikulu ya White House na kudaiwa kutumia vibaya nyaraka hizo nyeti za serikali.
Aidha, pia alithibitisha habari hizo kwenye ukurasa wa mtandao wake wa True Social, ambapo mawakili wake walimuarifu kuwa wizara ya sheria imemfungulia mashtaka na kwamba ametakiwa kujiwasilisha mbele ya Mahakama ya Miami.
Hata hivyo, baadhi ya maafisa wanaofahamu kesi hiyo, wamenukuliwa wakisema kwamba amefunguliwa mashtaka kadhaa ya uhalifu na hatua hiyo inamfanya Trump kuwa rais wa kwanza wa zamani kushtakiwa na Mahakama ya serikali kuu.