Imeelezwa kuwa meneja wa klabu ya Manchester City Pep Guardiola ana mpango wa kumsajili kiungo mshambuliaji kutoka England na klabu ya Aston Villa Jack Peter Grealish.
Guardiola anatajwa kuwa kwenye mpango huo, baada ya kusaini mkataba mpya wa kuendelea kuitumikia Manchester City kama mkuu wa benchi la ufundi kwa miaka miwili zaidi.
Taarifa zinaeleza kuwa meneja huyo kutoka Hispania amekiri wazi kuwa kikosi chake kinahitaji mabadiliko makubwa, na tayari ana orodha ya wachezaji anaotamani kuwasajili kwa msimu ujao wa Ligi Kuu ya England.
Jack Grealish, Harry Kane na Lionel Messi ni majina makubwa yanayopewa kipaumbele kwenye orodha ya wachezaji wanaohitajika na Guardiola katika kuunda kikosi kipya.
Gazeti la Independent limeandika kuwa Guardiola ameshawasilisha orodha hiyo kwa uongozi wa juu, na kwa sasa anasubiri baraka kutoka kwa mabosi wake.
Kevin De Bryune anatajwa kuwa miongoni mwa wachezaji waliopendekeza jina la Grealish na walifanya mazungumzo ya kina na Guardiola kabla ya kuufikia uongozi wa Manchester City na kuwaelekeza kufanya hivyo mapema iwezekanavyo.
Kwa upande wa Grealish, inaaminika watu waliopo karibu na mchezaji huyo wanaamini ni suala la muda tu tukizungumzia mchezaji huyo kujiunga na timu yeyote kubwa kwenye akitokea Aston Villa ambapo ndiyo timu aliyoanzia maisha yake ya soka na yupo hapo mpaka sasa.
Licha ya Manchester City kuhusishwa na Messi, Pep Guardiola alinukuliwa akimsihi mchezaji huyo kuendelea kubaki FC Barcelona na taarifa zilizopo ni kuwa timu hiyo imejiondoa katika mchakato wa kumsajili Messi kutokana na umri wake (33) na mshahara wake ni mkubwa (Pauni Milioni 100 kwa mwaka).