Beki kutoka nchini Ivory Coast, Mohammed Ouattara amelazimika kuondolewa kwenye kikosi cha Simba SC, kinachoendelea maandalizi ya mchezo wa Mzunguuko watano wa Kundi D, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Mabigwa wa Guinea Horoya AC.
Simba SC itakua mwenyeji wa mchezo huo unaosubiriwa kwa hamu kubwa na Mashabiki na Wanachama wa Klabu hiyo, Jumamosi (Machi 18) katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, huku ikihitaji ushindi ili kufuzu Robo Fainali.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally amesema Ouattara ameondolewa kambini sambamba na kupewa mapumziko ya siku tatu baada ya kupata maumivu akiwa mazoezini.
“Ouattara amepewa mapumziko ya siku tatu baada ya kuumia, hivyo ameondolewa katika kikosi kinachojiandaa na mchezo dhidi ya Horoya AC.
“Wakati Ouattara akiwa nje akiuguza maumivu yake, kiungo wetu Sawadogo (Ismael) yeye ameanza mazoezi mepesi ya binafsi katika kujiandaa na mchezo huo dhidi ya Horoya AC.
“Hivyo yupo chini ya uangalizi maalum wa madaktari ambao hivi sasa wanaendelea kumpa matibabu ili kuhakikisha anarejea uwanjani mapema,” amesema Ally
Wakati Simba SC inaelekea katika mchezo dhidi ya Horoya AC, tayari imeshajikusanyia alama 06 zinazoiweka nafasi ya pili katika msimamo wa Kundi C, linaloongozwa na Raja Casablanca ya Morocco yenye alama 12.
Horoya AC inashika nafasi ya tatu katika Kundi hilo ikiwa na alama 04, na Vipers SC ya Uganda inaburuza mkia ikiwa na alama 01.