Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Franco Pablo Martin amesema mikakati yao kwenye mchezo wa Fainali ya Mapinduzi 2022 dhidi ya Azam FC ni kuhakikisha wanashinda na kutwaa ubingwa.
Mchezo wa leo utakuwa wa ushindani mkubwa ikiwa kila upande una malengo yake, kuhitaji kuondoka na Kombe la Mapinduzi.
Kocha huyo kutoka nchini Hispania amesema wamejiandaa vizuri kuelekea mchezo huo utakaoanza mishale ya saa Mbili na Robo usiku, huku akisisitiza wachezaji wako fiti na tayari kwa ajili ya kupambana kuhakikisha wanafikia malengo yao ya kulibeba taji hilo.
“Wachezaji walicheza kwa kiwango bora sana dhidi ya Namungo FC, nina matarajio makubwa kwa mchezo wa leo, utakuwa mzuri na ushindani mkubwa kwa wenzetu na kwetu pia.”
“Azam FC ina wachezaji wazuri na wanapambana kutafuta matokeo, tumeona ubora wao na kuufanyia kazi, tuna waheshimu, tutacheza kwa tahadhari ili kufikia malengo yanayotarajiwa wa wana Simba wote,” amesema Pablo.
Simba SC ilitinga Fainali ya Mapinduzi 2022 kwa kuifunga Namungo FC mabao 2-0, yaliyofungwa na Mshambuliaji kutoka nchini Rwanda Meddie Kagere na Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Senegal Pappe Ousman Sakho.