Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), imewatimua watendaji wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kutokana na kutofika kikaoni kwa maofisa masuuli waliopaswa kujibu hoja za ukaguzi mbele ya Kamati hiyo iliyofanya kikao Bungeni jijini Dodoma.
Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya PAC Naghenjwa Kabayoko wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya Kamati hiyo kukutana Bungeni jijini Dodoma na kuongeza kuwa wameadhimia kutowaita tena maofisa masuuli hao, ambao hawajali maazimio ya Bunge.
Amesema ukaguzi huo ulifanyika kwa hesabu za miaka mitano za taasisi hizo kuanzia mwaka 2016 hadi mwaka 2021, ulilenga ni kubaini fedha zilizopotea kutokana na mambo mbalimbali ikiwemo mikataba mibovu na kwamba aliyefika mbele ya kamati hiyo ni Naibu Katibu Mkuu wa Ujenzi tu ambaye kisheria siyo ofisa masuhuli anayetakiwa kuwajibika mbele ya kamati.
Amesema, “kutokana na hayo basi kamati yangu imeadhimia kuwa kwa vile maofisa masuuli ambao leo ndiyo ilikuwa tuwaambie kauli yetu ya mwisho hawakuwepo na kwamaana hiyo hakuna wa kumtuma tukaona hakuna haja ya kuendelea kufanya majadiliano maaan majibu yangekuwa ni yale yale na wangerudi kufanya matendo yale yale ambayo hawajali kuangalia kuwa maazimio ya bunge yanafanyiwa kazi kikamilifu.”
Aidha, ameongeza kuwa kwasasa hawatarajii kuziita tena taasisi hizo na badala yake watapeleka ripoti bungeni ili bunge lifanye maamuzi na kwamba anaamini Bunge halitakubali kuendelea kudharauliwa kwasababu kazi kubwa za bunge ziko mbili kuisimamia serikali na kuishauri.
Jumla ya Kamati 15 za kudumu za Bunge, zinaendelea na vikao vyake jijini Dodoma ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mkutano wa 10 wa Bunge unaotarajiwa kuanza Januari 31 mwaka huu (2023).