Hatimaye siku ya siku imefika! Usiku wa leo wababe Canelo ‘Saul’ Alvarez na Gennady ‘GGG’ Golovkin watakata mzizi wa fitna katika pambano lao la marudiano kufuta matokeo ya sare ya pambano la kwanza.
Pambano hili ambalo lina kila sifa ya kuitwa ‘Pambano la Mwaka’ kwa kuangalia ratiba ya mapambano mengi makubwa mwaka huu, limetawaliwa na kauli nzito na mgogoro mkubwa kati ya timu mbili za wapiganaji hao.
Tofauti na ilivyokuwa kwenye pambano la kwanza, maneno ya dharau na kutambiana yametawala zaidi hasa kufuaita tukio la Canelo kukutwa akiwa ametumia ‘dawa’ ambazo haziruhusiwi mchezoni miezi kadhaa iliyopita.
Canelo na timu yake wamemalizana na Mamlaka zinazosimamia mchezo wa masumbwi, na idara ya Nevada inayoshughulikia vipimo na afya ya mabondia na sasa yuko tayari kwa pambano.
Bondia huyo kutoka Mexico ameahidi kumzimisha GGG katika raundi ya kwanza ya pambano.
“Bila shaka, naenda kumpiga kwa KO, na hilo ndilo nilikuwa nalifanyia kazi kwenye mazoezi. Ninaenda kulitekeleza kuanzia raundi ya kwanza kumaliza lengo langu ambalo ni kumpiga kwa KO,” Canelo aliiamba TMZ.
Kwa upande wa GGG kutoka Kazakhstan, amesema kuwa atashinda pambano hilo na kwamba pamoja na kujiandaa vizuri, asilimia 80 ya mashabiki wanamuunga mkono na kumpa nguvu.
“Najisikia kuwa watu wengi hata wa Mexico (kwao Canelo) na dunia nzima kwa ujumla, asilimia 80 wananiunga mkono. Na nitarudisha mkanda wa ushindi nyumbani,” alisema.
“Pambano la kwanza lilikuwa kama majaribio lakini pambano la pili ni kubwa zaidi na linamvuto zaidi. Niko tayari,” aliongeza GGG.
Mabondia hao wamepima uzito jana usiku lakini taharuki iliibuka baada ya kusogeleana, tofauti na ilivyokuwa kwenye pambano la kwanza.
GGG ana rekodi ya kutopoteza pambano hata moja kati ya mapambano 39, akitoa sare ya pambano moja tu.
Wakati Canelo ana rekodi ya kupigana mapambano 52, akishinda mapambano 49, kushindwa moja na kutoa sare mapambano mawili.