Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis amechapisha Waraka mpya wa Kitume, akitoa wito wa kuwepo mshikamano katika jamii ili kuweza kuyashughulikia matatizo ya ulimwengu.
Katika waraka huo wa Kipapa uliopewa jina ”Fratelli Tutti”, yaani ”Sote ni Ndugu,” na kutolewa jana katika Uwanja wa Mtakatifu Peter, Vatican City umezikosoa sera za kinadharia kuhusu soko la kibepari kama suluhisho pekee la matatizo ya dunia.
Papa Francis amegusia matatizo ya dunia kama vile mabadiliko ya tabia nchi, dhuluma zinazosababishwa na ukosefu wa usawa wa kiuchumi, tatizo la wahamiaji na janga la virusi vya corona.
Waraka wa Kitume ni moja ya njia ya mawasiliano muhimu ya Papa na hutumika kama msingi wa mafundisho ya Kanisa Katoliki kwa kuangazia msimamo kuhusu masuala muhimu.