Klabu ya Paris Saint-Germain imetangazwa kuwa bingwa wa Ufaransa, msimu wa 2019/20, licha ya ligi ya nchi hiyo kusaliwa na zaidi ya michezo kumi.
Ligi ya Ufaransa ilisimamishwa kupisha vita dhidi maambukizo ya Virusi Vya Corona, huku mabingwa hao wakiwa wamecheza michezo 27 na kufikisha alama 68.
Kwa mujibu wa taarifa zilizochapishwa na gazeti la L’Equipe, Paris Saint-Germain wanakuwa mabingwa wa ligi ya Ufaransa, baada ya Serikari ya nchi hiyo kutangaza kufuta ligi zote kwa msimu huu 2019-20.
Maamuzi ya klabu hiyo kutawazwa kuwa mabingwa wa Ufaransa, pia yametoa nafasi kwa klabu za mkiani mwa msimamo wa ligi ya msimu huu kushushwa daraja na msimu ujao zitashiriki ligi daraja kwa pili (Ligue 2).
Klabu zilizoathiriwa na janga la kushuka daraja ni Amiens (Alama 23) na Toulouse (Alama 13) huku Nimes (Alama 27) inayoshika nafasi ya tatu kutoka chini ikisubiri kucheaza michezo ya mtoano kujihakiishia kubaki ama kushuka.
Kwa maamuzi hayo ya Serikali Paris Saint-Germain, Marseille na Rennes zitaiwakilisha Ufaransa kwenye michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya msimu ujao, huku Lille, Reims na Nice zikipata nafasi ya kushiriki michuano ya Europa League.
Klabu za FC Lorient na RC Lens, zimepata mbeleko ya kupandishwa daraja kutoka ligi daraja la pili (Ligue 2) na msimu ujao 2020-21 zitashiriki ligi darala la kwanza (Ligue 1).
Paris Saint-Germain wanakuwa mabingwa wa ufaransa kwa mara ya tatu mfululizo (2017–18, 2018–19 na 2019/20) huku wakitwaa taji hiyo kwa mara ya tisa kihistoria (1985–86, 1993–94, 2012–13, 2013–14, 2014–15, 2015–16, 2017–18 na 2018–19).