Wapinzani wa mabingwa wa soka Tanzania Bara Simba SC, kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika Plateau United, wanatarajiwa kuwasili jijini Dar es salaam leo mchana wakitokea nchini kwao Nigeria.
Plateau United ambao walipoteza mchezo wa mkondo wa kwanza dhidi ya Simba SC mjini Jos- Nigeria mwishoni mwa juma lililopita, walianza safari ya kuja Tanzania jana jioni kwa saa za Afrika Mashariki.
Wenyeji wao Simba SC wamethibitisha taarifa za ujio wa timu hiyo, ambayo inashiriki kwa mara ya kwanza michuano ya Klabu Bingwa Barani Afrika, tangu ilipoanzishwa mwaka 1975.
Wakati Plateau United wakitarajiwa kuwasili nchini baadae leo Ijumaa (Desemba 04), Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Simba SC, Haji Manara amesema maandalizi na taratibu zote za kiitifaki kuelekea mchezo wa kesho Jumamosi zimekamilika.
“Kutakuwa na taratibu zote zinazohusiana na COVID 19, naomba hili tulizingatie wote, tutaweka vitakasa mikono kwenye mageti yote, ni muhimu tuvae barakoa, wenzetu bado hili gonjwa wanalo, hapa wakifika wanatushangaa,” Alisema Manara alipozungumza na waandishi wa habari juzi Jumatano, jijini Dar es salaam.
Simba itawakaribisha Wanigeria hao kesho Jumamosi (Desemba 05), Uwanja wa Benjamin Mkapa, huku ikiwa na kumbukumbu ya kupata ushindi wa bao moja kwa sifuri, walioupata kwenye uwanja wa New Jos, Nigeria mwishoni mwa juma lililopita. Bao hilo pekee lilifungwa na kiungo kutoka nchini Zambia Clatous Chama.