Kocha mpya wa The Blues Mauricio Pochettino ameripotiwa kuwa na mpango wa kupiga bei mastaa wanne kwenye kikosi chake kabla ya maandalizi ya msimu mpya hayajaanza juma lijalo.
Chelsea imeshawaondoa mastaa kadhaa kwenye kikosi chao katika dirisha hili akiwamo Mateo Kovacic, Kai Havertz, Edouard Mendy, N’Golo Kante na Kalidou Koulibaly.
Lakini, bado kuna wachezaji wengine wanaohitaji kuondoka kwenye kikosi hicho Romelu Lukaku, Hakim Ziyech, Christian Pulisic na Pierre-Emerick Aubameyang na kocha Pochettino ana kazi ya kuwaondoa wachezaji hao kabla hajaanza rasmi mazoezi ya kukifuma kikosi chake kwa ajili ya msimu ujao.
Wakati wakiwa bado hawajapata timu, Pochettino anakuna kichwa kama ama awaaondoa kwenye kikosi chake, wafanye mazoezi kivyao, wakati wakitarajia kuanza kujifua Cobham, Jumatano ijayo.
Mastaa hao wanne wanaweza kuweka kando kwenye ziada ya Pre-Season ya timu hiyo iliyopangwa kufanyika huko Amerika kuanzia Julai 17.
Kuna uwezekano pia wakawekwa kwenye kundi la timu B na kufanya mazoezi huko, wakati kikosi cha kwanza kikipiga kambi huko Marekani.
Pochettino yupo na kazi nzito ya kurudisha makali ya Chelsea baada ya kumaliza nafasi ya 12 kwenye msimamo wa Ligi Kuu England msimu uliopita.