Wajumbe 1876 wa mkutano mkuu maalumu wa CCM wanatarajiwa kupiga kura jina moja litakalowasilishwa katika mkutano huo kumchagua mwenyekiti mpya wa chama hicho tawala nchini.
Mkutano huo unafanyika baada ya aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho, rais wa awamu ya tano, Hayati John Magufuli kufariki dunia Machi 17,2021 na atakayechaguliwa kuwa mwenyekiti mpya ni Rais Samia Suluhu Hassan.
Kwa mujibu wa katiba ya chama hicho baada ya kifo cha Magufuli, mchakato wa kumpata mwenyekiti mwingine ziliendelea kufanyika na kesho ndio unafanyika uchaguzi huo.
Akizungumza leo Alhamisi Aprili 29,2021 kuhusu maandalizi ya mkutano huo katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, Humphrey Polepole amesema wajumbe kutoka sehemu mbalimbali watashiriki mkutano huo.
Amesema mbali na wajumbe hao ambao watashiriki kupiga kura, wapo wageni 1,000 watakaoshiriki mkutano wakiwamo kutoka vyama mbalimbali vya siasa nchini, wawakilishi wa vyama rafiki vilivyoshiriki katika ukombozi wa Bara la Afrika na mabalozi.
Amebainisha kuwa mkutano huo utaongozwa na makamu mwenyekiti wa CCM- Bara, Philip Mangula na makamu mwenyekiti wa chama hicho Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein.