Raia na wanaharakati wa mashirika ya kiraia wameingia mitaani nje ya Kurugenzi ya Polisi katika mji mkuu wa Albania, Tirana kupaza sauti juu ya tukio la ubakaji linalotunikwa alilofanyiwa msichana kutoka Kenya.
Msichana huyo, Joy Aoko (22), alipatikana akiwa amepoteza fahamu chini ya jengo alilokuwa akiishi jijini Tirana mnamo Agosti 13, 2022 na wanaharakati hao kwa pamoja na raia wanadai haki na kuwashutumu Polisi kwa kutochukua hatua stahiki.
Akizungumza na umati wa watu, mwanaharakati Xheni Karaj alihoji “Je, haki inafanya kazi kwa watu wabaya pekee? Kufunika uhalifu huu kunaweka historia dhidi ya wanyonge katika nchi nzima, sisi tunadai uchunguzi mkali ufanyike na tunataka wahusika wafikishwe mahakamani.”
Xheni ameendelea kueleza kuwa, Taasisi husika zinatakiwa zilipe bili ya matibabu yake nje ya nchi huku Wakili, Idajet Beqiri aliyekuwa sehemu ya waandamanaji akisema alikasirishwa Polisi kuficha tukio hilo akidai huo nao ni uhalifu.
Alisema, “Ni aibu kubwa kwa taasisi za Albania, tukio hili lilitokea Agosti 14 na polisi hawakuwajulisha raia Polisi wa serikali walificha uhalifu, Je, hii yote ni kuhusu ubaguzi wa rangi au kuna sababu nyingine? Kufunika uhalifu yenyewe pia ni uhalifu.”
Mama mzani wa Joy, Ruth Aoka, hakuwa sehemu ya maandamano hayo lakini katika mahojiano alisema msichana huyo alikuwa akifukuzwa na dereva wa kasino kwa muda mrefu na kwamba alihisi kutishiwa maisha na hayuko salama huku Ofisi ya mwendesha mashtaka ikisema tayari imeanza uchunguzi kuhusu tukio hilo lakini bado hakuna jibu la nini hasa kilimpata Joy.