Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam imezuia mkutano kati ya waandishi wa habari na Kiongozi wa ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe ambao ulitarajiwa kufanyika leo Ijumaa Agosti 16, 2019 saa 5 asubuhi.
Polisi waliwasili Makao Makuu ya chama hicho cha upinzani yaliyopo Kijitonyama jijini Dar es salaam na gari wakiwa wamevaa nguo za kiraia na kuzuia mkutano huo na baadaye gari ya polisi waliokuwa na sare waliwasili na kumhitaji kiongozi yoyote wa chama baada ya kumkosa Zitto.
“Ndugu waandishi huu mkutano usubiri kwanza, kwa hiyo ninawaomba mtawanyike mara moja,” amesema askari mmoja aliyejitambulisha kama RCO wa Kinondoni, John Malulu.
Wakati waandishi wakitawanyika aliwasili Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mawasiliano wa ACT- Wazalendo, Ado Shaibu ambaye wamemchukua kwa ajili ya mahojiano.
Hata hivyo, kabla ya kuchukuliwa na polisi, Ado Shaibu amesema polisi walikwenda nyumbani kwa Zitto kumtafuta kwa ajili ya kumhoji.
“Zitto alitaka kuzungumzia kuhusu mkutano wa (Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika) SADC unaoendelea hapa nchini lakini wameniambia niondoke nao kwenda polisi, hawajaniambia ni kituo gani, nimewaambia ngoja niweke mambo sawa kisha tuondoke wote, hamna haja ya kuwa na wasiwasi,” amesema Shaibu.
Polisi wamemchukua, Ado Shaibu kwa ajili ya mahojiano. lakini kwa upande wa polisi wamekataa kuzungumza kuhusu sababu za kuzuia mkutano huo.