Jeshi la Polisi Nchini kenya wamefukua maiti 10 kutoka katika makaburi ya halaiki yanayohusishwa na ibada ya njaa na kufanya jumla ya waathirika kufikia 83 katika msitu wa Shakahola karibu na mji wa Pwani wa Malindi mara baada ya kupokea taarifa kuhusu dhehebu linaloongozwa na Paul Mackenzie Nthenge, ambaye aliwataka wafuasi wake kufa njaa ili kumtafuta Mungu.

Kwa mujibu wa Ctizen Digital na mwandishi wa AFP amesema kuwa jumanne miili ya watu kumi ilipatikana ikijumuisha watoto watatu, huku waokozi wakifukua mabaki yao kutoka kwenye makaburi yasiyo na kina kirefu na pia waliwakuta manusura wawili wakiodhoofika.

Ugunduzi huo mbaya umeleta mshtuko kote nchini, na kumfanya Rais William Ruto kuahidi kukandamiza mienendo ya kidini isiyokubalika.

Huku vifo hivyo vikiongezeka, mamlaka katika hospitali ya Serikali ya Kaunti Ndogo ya Malindi ilionya kwamba chumba cha kuhifadhia maiti kilikuwa kinakosa nafasi ya kuhifadhi miili .

Msimamizi wa Hospitali hiyo Said Ali alisema hospitali hiyo inauwezo wa kubeba miili 40, ambapo ameongeza kuwa maafisa walifika kwa Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya kwa ajili ya makontena yaliyohifadhiwa kwenye jokofu.

Inaaminika kuwa baadhi ya wafuasi wa Kanisa la Good News International bado wanaweza kujificha msituni karibu na Shakahola na kuwa katika hatari ya kifo iwapo hawatapatikana haraka.

Inspekta Jenerali wa Polisi Japhet Koome aliwaambia wanahabari siku ya Jumatatu kuwa watu 29 wameokolewa na kupelekwa hospitalini.

Waziri wa Mambo ya Ndani Kithure Kindiki ametangaza mipango ya kuzuru eneo hilo siku ya Jumanne, huku Ruto akiapa kuwachukulia hatua wachungaji walaghai kama Nthenge “wanaotaka kutumia dini kuendeleza itikadi za ajabu na zisizokubalika”, akiwalinganisha na magaidi.

Huku viongozi wa Kenya wakijaribu kufichua ukubwa halisi wa kile kinachoitwa “Mauaji ya Msitu wa Shakahola”, maswali yameibuka kuhusu jinsi dhehebu hilo liliweza kufanya kazi bila kutambuliwa licha ya Nthenge kuvutia polisi miaka sita iliyopita.

Mwinjilisti huyo wa televisheni alikamatwa mwaka wa 2017 kwa madai ya “itikadi kali” baada ya kuzitaka familia zisiwapeleke watoto wao shule, akisema elimu haitambuliwi na Biblia.

Nthenge alikamatwa tena mwezi uliopita, kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini humo, baada ya watoto wawili kufa njaa wakiwa chini ya ulinzi wa wazazi wao.

Aliachiliwa kwa dhamana ya shilingi 100,000 za Kenya ($700) kabla ya kujisalimisha kwa polisi kufuatia uvamizi wa Shakahola ambapo kesi hiyo inatarajiwa kutajwa Mei 2, 2023.

Rais Mwinyi asifu miaka 59 ya Muungano
Ujenzi mradi wa Umeme JNHPP wafikia asilimia 85.06