Rais wa Zanzibar ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema miaka 59 ya Muungano wa Tanzania imeleta Mapinduzi makubwa katika sekta ya Elimu kwa pande zote ikiwemo kuboresha miundombinu ya majengo ya kisasa.

Dkt. Mwinyi aliyasema hayo kwenye sherehe za ufunguzi wa Skuli ya msingi ya kisasa Kidongochekundu iliopo kwenye jimbo la Jang’ombe, Wilaya ya Mjini ikiwa ni shamrashamra za miaka 59 ya Muungano wa Tanzania.

“Skuli hii ni sehemu ya Maadhimisho ya miaka 59 ya muungano wa Tanzania yaani Tanganyika na Zanzibar April 26, 1964 waasisi wa taifa letu Hayati Mwl. Julius Nyerere na Hayati Abeid Amen Karume waliwaongoza wananchi wa nchi mbili hizi za Jamhuri ya watu wa Tanganyika na Jamhuri ya watu wa Zanzibar kufanya Muungano wa Tanzania” amesema Rais Mwinyi.

“Pamoja na mambo mengine madhumuni ya kuanzisha muungano huu ni kudumisha udugu wetu wa damu na wa kihistoria baina ya wananchi wa iliyokuwa Tanganyika na Zanzibar katika nyanja mbalimbali za maendeleo”

Aidha amesema kuwa Mabadiliko ya elimu Zanzibar yatafikiwa kwakuwa na ujenzi imara wa miundombinu ya kisasa yatakayochukua wanafunzi wachache kwenye madarasa vifaa vya kisasa na mazingira mazuri ya kufundisha na kujifunza.

”Maelengo ya Serikali ni kwamba wakati wa kutimiza miaka 60 ya Muungano wetu mwaka 2024 tuwe tumeweza kupunguza zaidi changamoto ya sekta ya elimu kwa kuongeza miundombinu ya skuli kwa kujenga madarasa 1000 kupitia bajeti ya mwaka 2023/2024, Serikali pia itazifanyia matengenezo makubwa skuli mbalimbali Unguja na Pemba ikiwemo skuli hii kongwe ya msingi ya hapa kidongochekundu”Amesema Rais Mwinyi.

Naye Waziri wa Elimu na mafunzo ya mali Leila Musa amesema ujenzi wa skuli hiyo ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya chama cha mapinduzi ya mwaka 2020/2025 ambapo Serikali ya Mapindizi Zanzibar iliahidi kujenga miradi mbalimbali ya maendeleo

Skuli ya msingi ya Kidongochekundu ni miongoni mwa skuli mpya zilizojengwa na Serikali ya awamu ya nane kwa fedha ya ahueni ya Uviko 19 Zanzibar kwa Unguja na Pemba

Bwawa la Mwalimu Nyerere kuwaneemesha Watanzania - Makamba
Polisi yafukua maiti 10 katika kaburi la Halaiki