Mhubiri mashuhuri nchini Kenya, Ezekiel Odero, amefikishwa katika Mahakama ya Shanzu mjini Mombasa akihusishwa na vifo vya miili ya watu zaidi ya 100 iliyofukuliwa katika shamba la Shakahola ambalo linamilikiwa na mhubiri mwengine Paul Mackenzie, ambaye pia anashikiliwa na polisi.
Mara baada ya kufikishwa mahakamani hapo, upande wa mashitaka uliomba mchungaji huyo ashikiliwe kwa siku zingine 30, ili kuweza kufanya uchunguzi na wa tuhuma za mauaji, utekaji wa watu, kuwatesa watoto, ulaghai, utakatishaji wa fedha na uenezaji wa itikadi kali.
Odero Maarufu kama Pastor Ezekiel anahusishwa na vifo vya wafuasi wake Picha ya REUTERS.
Odero Maarufu kama Pastor Ezekiel, anatuhumiwa kuwa mtu wa karibu wa Paul Mackenzie wa kanisa Good News International la Pwani ya Kenya ambaye pia anashikiliwa na maofisa wa polisi kwa makosa ya kuwataka wafuasi wake kufunga kula na kunywa hadi wafe.
Hata hivyo, wafuasi wa pasta Ezekiel, wamekusanyika nje ya majengo ya mahakama ya Shanzu wakiwa wamebeba Biblia mikononi wakiomba na kutatafuta msaada wa mwenyezi Mungu kwa kile anachokabiliwa nacho kiongozi wao wakisema shutuma dhidi yake hazina ukweli.