Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo, amepuuzia mbali matokeo ya uchaguzi wa Rais uliofanyika wiki iliyopita ambayo yalionyesha kuwa Rais Donald Trump ameshindwa.
Pompeo amewaambia waandishi habari kuwa kipindi cha mpito kuelekea muhula wa pili wa Trump kitatokea bila wasiwasi wowote na kwamba wizara ya mambo ya nje itakuwa tayari bila kujali nani atakayekuwa Rais wa Marekani ifikapo Januari 20, mwakani.
Kauli ya Pompeo kuashiria kuwa Trump anaweza kuhudumu tena kwa muhula wa pili, inakuja wakati ambapo Trump amekataa kukubali kushindwa na Rais mteule Joe Biden.
Trump anapanga kuwasilisha kesi mahakamani katika jimbo la Michigan ili kupinga matokeo ya uchaguzi katika juhudi zake za kusalia madarakani ikiwa ni siku moja tangu awasilishe kesi kama hiyo katika jimbo la Pennsylvania.
Kwa upande wake Rais mteule wa Marekani Joe Biden anapanga kufanya mikutano zaidi leo Jumatano ili kuweka msingi wa utawala wake.
Hata hivyo majaji wametupilia mbali kesi zilizowasilishwa katika majimbo ya Michigan na Georgia, huku wataalam wa kisheria wakisema madai hayo yana nafasi ndogo ya kubadilisha matokeo ya uchaguzi wa Novemba 3.