Mamlaka ya Kudhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA) imewahamasisha wanawake, vijana, wazee na watu wenye ulemavu kuchangamkia fursa ya asilimia 30 ya bajeti ya ununuzi ya Serikali inayotengwa kwa ajili yao kama makundi maalum.
Hamasa hiyo imetolewa na Afisa Uhusiano kwa Umma Mkuu wa PPRA, Bi. Zawadi Msalla alipozungumza na waandishi wa habari katika banda la Mamlaka hiyo kwenye Maonesho ya Wakulima maarufu kama Nanenane yanayofanyika kitaifa jijini Mbeya.
Bi. Msalla alisema kwa mujibu wa Sheria ya Ununuzi wa Umma Sura 410, taasisi zote nunuzi zinapaswa kutenga asilimia 30 ya bajeti ya ununuzi ya mwaka kwa ajili ya makundi maalum.
Alisema kiwango hicho kinachotengwa na Serikali ni fursa kubwa inayoweza kuwainua kiuchumi ikiwa ndiyo dhamira ya Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
“Hii ni fursa adhimu inayotolewa na Serikali na ikitumika ipasavyo tutaongeza wigo wa ajira. Ukichukulia mfano wa mwaka wa fedha uliopita, jumla ya bajeti ya ununuzi ya serikali ilikuwa takribani Sh. 22 trilioni, ambayo 30% ni takribani sh. 6.6 trilioni. Zabuni za thamani hii zote zilitengwa kwa ajili ya makundi maalum. Kwa mwaka huu tunaamini itaongezeka,” alisema Bi. Msalla.
Akirejea hotuba ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Tanzania, Dkt. Philip Mpango alipokuwa akifungua maonesho hayo, kuwa kumekuwa na mwamko unaoridhisha wa mabenki ya biashara kutoa mikopo kwenye sekta ya kilimo, Bi. Msalla alisema hatua hiyo itawezesha upatikanaji wa mitaji zaidi, na makundi maalum wanaweza kitumia mitaji hiyo katika fursa ya zabuni za umma.
“Kwa bahati nzuri Serikali kupitia Halmashauri na Ofisi ya Waziri Mkuu inatoa mikopo ya riba nafuu kwa makundi haya. Lakini pia, kama alivyosema Mheshimiwa Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango mabenki pia yanaongeza nguvu ya mikopo kwenye sekta ya kilimo ambapo huko nako ziko tenda za Serikali. Kwakuwa wigo wa kupata mikopo umeongezeka, wanaweza kufanya biashara na serikali kwa nafasi hii ya kutumia asilimia 30 zlizotengwa na taasisi hizo za kilimo,” aliongeza Bi. Msalla.
Akieleza jinsi ya kutambulika kama kundi maalum kwa ajili ya zabuni za umma, Bi. Msalla alisema baada ya kuunda kikundi wanapaswa kusajiliwa na taasisi wezeshi kama Halmashauri, Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO), Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) n.k. Kabla ya kusajiliwa watapewa mafunzo maalum kuhusu ununuzi wa umma pamoja na usimamizi wa fedha.
Alifafanua kuwa baada ya usajili huo jina la kikundi husika litawasilishwa PPRA na kuwekwa kwenye orodha mahsusi ya makundi maalum, kisha wanaweza kushiriki michakato ya kupata asilimia 30% ya zabuni. Taarifa zilizowekwa kwenye tovuti ya PPRA zinaonesha kuwa hadi Agosti 3, 2022 jumla ya vikundi 181 tu ndivyo vilivyosajiliwa kama makundi maalum kwa nchi nzima.