China imesema itafanya kazi kwa ukaribu na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mara baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu ili kuiwezesha Tanzania kupiga kwa haraka hatua za kimaendeleo kwa faida ya pande zote mbili.
Hayo yameelezwa katika barua ya pongezi iliyotumwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi kwenda kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi iliyowasilishwa kwake na Balozi wa China nchini, Wang Ke.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi barua hiyo, Balozi Wang Ke amesema China ina imani na serikali ya Tanzania hususan mara baada ya uchaguzi mkuu uliomalizika mwezi Oktoba kwa utulivu na amani na kwamba imejipanga kuimarisha mahusiano ya kimkakati ili kuwaletea wananchi maendeleo.
Kwa upande wake Prof. Kabudi amesema anazipokea kwa unyenyekevu salamu hizo za pongezi kutoka kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi, na kuongeza kuwa katika mazungumzo yake na Balozi Wang Ke wameangazia masuala mbalimbali ya kimkakati ya kutekeleza, hususan yale yanayolenga katika hotuba ya Rais wa Tanzania Dkt. John Magufuli wakati akilifungua Bunge la 12, jijini Dodoma.
Katika hatua nyingine, Prof. Kabudi amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Sweden nchini Anders Sjoberg, na baadae kukutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Finland nchini Riitta Swan.