Serikali imeshauriwa kujiridhisha na umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia na iwapo imejipanga kukabili madhara yanayoweza kujitokeza ya watu kukosa ajira na kufa kwa viwanda vidogovidogo vya uzalishaji nchini.
Hayo yamebainishwa na Mshiriki wa mjadala wa Kitaifa wa Nishati safi ya kupikia Prof. Ishengoma hii leo Novemba 2, 2022 jijini Dar es Salaam na kuongeza kuwa ipo haja ya kujiuliza swali Nishati safi ya kupikia ni ipi licha ya kwamba ina mambo mengi mazuri lakini ambayo si salama.
Amesema, “Mimi leo nawachokoza na hoja zangu je unataka tuhamie kwenye gesi ni sawa lakini kuhama huku unaharibu ajira za watu wangapi, na baada ya hapo watu hawa watafanya nini na je nishati safi ya kupikia ni ipi haya ni mambo ya msingi ya kujiuliza.”
Ishengoma ameongeza kuwa, ni vyema kutoa mwelekeo wa suala hilo na kutazama aina ya kipindi cha mpito kitakachokuwa na matazamio, kwani zipo faida na hasara za uamuzi wa matumizi rasmi ya nishati safu na kutolea mfano vita ya Ukraine ambavyo vimeathiri upatikanaji wa gesi na hivyo watu kuwa na wakati mgumu.
“Si mmeona wenyewe vita ya Ukraine ilivyoathiri matumizi ya gesi, niambieni hawa watu hawatumii kuni kwasasa, wamesharudia uasili hatukatai gesi ni nzuri lakini ni lazima kuangalia misingi ya awali ilipotutoa na wapi tunakwenda,” ameongeza Ishengoma.
Hata hivyo, amesema wakati huu ambao Serikali ipo katika uhimizaji wa matumizi ya nishati safi ya kupikia ni vyema ikaangalia masuala ya usafirishaji wa mitungi ya gesi na mazingira yake kiusalama majumbani na kutazama fursa za upatikanaji wa gesi ya hapa nchini na si kuwanufaisha wageni.