Katibu Mkuu Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Profesa Kitila Mkumbo amezungumzia taarifa zilizosambaa mitandaoni kuwa anapanga kushiriki kinyanyiro cha uchaguzi wa Ubunge wa Singida Kaskazini, kuziba nafasi ya Lazaro Nyalandu aliyejiuzulu na kuhamia Chadema.
Profesa Kitila ambaye hivi karibuni amejiunga rasmi na CCM, amesema kuwa hana mpango wa kugombea katika jimbo hilo.
“Kugombania jimbo ni mpango, unaamua mwenyewe. Lakini kwakweli sina mpango wa kugombea kwenye jimbo hilo la Nyalandu,” Profesa Kitila ameiambia Clouds FM.
Hata hivyo, amesema kuwa waliotoa tetesi hizo wana haki ya kuhisi kwani kuhisi sio kupakazia na kwamba anaamini wamemuona anafaa.
Profesa Kitila ambaye alikuwa mshauri mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo alitangaza kujiunga rasmi na CCM hivi karibuni.
Mbali na Mkumbo, aliyekuwa mwanasheria wa ACT Wazalendo, Alberto Msando na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema, Patrobas Katambi ambao pamoja na Laurent Masha; na Samson Mwigamba walijiunga rasmi na CCM katika kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho (NEC- CCM), unaoendelea Ikulu jijini Dar es Salaam.