Mbunge wa Muleba Kusini, Profesa Anna Tibaijuka (CCM) ametangaza kung’atuka nafasi ya Ubunge itakapofika mwaka 2020.

Profesa Tibaijuka ambaye alikuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi katika Serikali ya Awamu ya Nne na baadae kujiuzulu nafasi hiyo kufuatia sakata la Escrow, amesema kuwa tayari ameshawaaga wananchi wake ambao wanamuamini.

Amesema kuwa lengo la kutokugombea tena nafasi hiyo ni kuwapa nafasi vijana ili waongoze nchi kwani yeye amefanya kazi hiyo kwa muda mrefu.

“Sisi ni watu wazima. Kizazi chetu tumeshamaliza kazi. Tumeshastaafu. Na mimi nikimaliza ubunge muhula huu nastaafu,” Profesa Tibaijuka aliiambia TBC.

“Kuzeeka haimaanishi kwamba maarifa yangu yameondoka kwa sababu nimestaafu, napenda tuwape nafasi vijana washike nchi,” aliongeza.

Mwanasiasa huyo mkongwe alimnukuu Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kuwa alisema ‘watu wang’atuke’, hivyo na yeye anang’atuka ili maarifa yake ayatumie kutoa ushauri.

Profesa Tibaijuka amekuwa mbunge wa Muleba tangu mwaka 2010, na kutumikia nafasi ya Uwaziri wa Ardhi kuanzia mwaka huo hadi mwaka 2014 alipolazimika kujiuzulu.

Video: Bomu mkono lilivyoua wanafunzi..., Kashfa nzito vigogo sukari
RPC Kagera azungumzia chanzo cha mlipuko wa bomu