Mamlaka ya Udhibiti mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), imesema takribani kilomita za mraba 534,000 zimefanyiwa tafiti, ili kubaini juu ya uwezekano wa kupatikana kwa Mafuta na Gesi asilia, ambapo kati ya hizo, kilomita za mraba 394,000 tafiti yake imefanyika nchi kavu, wakati kilomita za mraba 140,000 tafiti yake imefanyika upande wa Baharini.
Wakati Tafiti hizo zikifanyika Mamlaka hiyo imesema mpaka Sasa Gesi asilia iliyogunduliwa nchi Kavu ni Futi za Ujazo Trilioni 10.41, wakati kwenye kina kirefu cha Bahari ikiwa ni Futi za Ujazo Trilioni 47.13.
Ripoti hiyo imebainishwa Novemba 06, 2023 Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Mhandisi Charles Sangweni katika Wasilisho lake kwenye kikao kazi kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina Nchini.
“Jumla ya Visima vya Utafutaji wa Mafuta vilivyochimbwa nchini ni 96 ambapo kati ya Visima hivyo, Visima 59 vipo nchi kavu wakati visima 37 vipo Baharini, aidha Gesi asilia imegunduliwa kwenye Visima 44, kwenye visima 96 vilivyochimbwa Nchi Kavu na Kwenye Kina cha Bahari” amesema Sangweni.
Aidha, Mhandisi Sangweni amebainisha kuwa kwa sasa Wastani wa Uzalishaji Gesi asilia umeongezeka na kufikia Futi za Ujazo Bilioni 53.19 katika Kipindi cha Julai 2022 hadi Februari 2023 ikilinganishwa na Futi za Ujazo Bilioni 46.96 mwaka 2021/2022 sawa na Ongezeko la asilimia 14.
“Ugunduzi na Uzalishaji Gesi asilia umewezesha itumike maeneo mbalimbali, ikiwemo uzalishaji Umeme, matumizi ya Viwandani, Majumbani na kwenye magari, ambapo kiasi cha Gesi iliyozalishwa imechangia asilimia 70 ya Umeme hapa unaopatikana nchini” amefafanua Mhandisi Sangweni.
Kwasasa maeneo ambayo Gesi asilia imegundulika nchini ni pamoja Songo Songo, Mnazi bay, Mkuranga, Kiliwani Kaskazini, Ntorya, Ruvu pamoja na Kwenye Kina Kirefu cha Bahari.
Taasisi ya Udhibiti wa Shughuli za mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), ilianzishwa mwaka 2015 kupitia Sheria ya Petroli, ambapo ilianza Shughuli zake Februari 2016 ikiwemo kuishauri Serikali kuhusu Shughuli za mkondo wa Juu wa Petroli kwa maana ya mafuta na Gesi, kudhibiti na Kusimamia Shughuli za Mkondo wa Juu wa Petroli pamoja na miradi ya Kubadili Gesi kuwa katika hali ya Kimiminika.