Aliyekuwa Mbunge wa Tabora Mjini, Ismail Rage, ameupongeza uongozi wa timu ya Tabora United kwa kusajili wachezaji wenye uwezo mkubwa wa kucheza soka la ushindani.

Rage ambaye pia aliwahi kuwa Mwenyekiti wa klabu ya Simba SC, amesema kiwango na matokeo ambayo timu hiyo imeyapata katika mechi tano za ligi walizocheza yanadhihirisha namna walivyojipanga kutoa upinzani msimu huu.

“Nawapongeza viongozi wa Tabora United, wametengeneza timu nzuri na benchi la ufundi imara sana kwa matokeo na nafasi waliyopo kwenye msimamo katika mechi tano walizocheza inaonesha wamekuja kushindana siyo kuzisindikiza Simba SC na Young Africans,” amesema Rage.

Kiongozi huyo amesema ameshuhudia mechi mbili za timu hiyo wakiwa nyumbani Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi ameona namna wachezaji na Kocha Mkuu, Goran Kopunovic wanavyojituma kutafuta ushindi kitu ambacho hakipatikani kwa baadhi ya timu kubwa nchini.

Amesema kwa ari ya upambanaji waliyonayo Tabora, timu nyingi zikiwemo Simba SC na Young Africans zijipange ikiwemo kujiandaa kupoteza mchezo.

Rage amesema kama timu hiyo itaendelea hivyo anaamini kuna uwezekano ikamaliza nafasi nne za juu na mwakani ikawakilisha taifa kwenye michuano ya kimataifa.

Tabora United inashika nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na pointi nane katika mechi tano walizocheza hadi sasa.

Tite akabidhiwa jukumu Flamengo
Sanaa: Wasanii wenye sifa waitwa kupewa Mkopo