Aliyewahi kuwa Mwenyekiti Simba SC Ismail Aden Rage amemuonya Kiungo kutoka visiwani Zanzibar Feisal Salum ‘Fei Toto’ akikata Rufaa Mahakama ya usuluhishi wa Michezo ‘CAS’ atakuwa anapoteza muda tu.
Wanasheria wa kiungo huyo aliaahidi kwenda mbele kusaka haki ya Mteja wao, baada ya Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya ‘TFF’ kumtaka kurejea Young Africans, kufuatia Mkataba wake kuwa halali kisheria.
Rage amemtaka ‘Fei Toto’ akae chini na Uongozi wa Young Africans ili kusaka suluhu, badala ya kukimbilia CAS kwani maamuzi ya Kamati ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji kuwa yeye ni mchezaji halali wa Young Africans hayawezi kutenguliwa huko.
“Unapotaka kufungua kesi CAS kwanza uwe na hakika sheria za FIFA zimevunjwa, sasa hili la ‘Fei Toto’ hakuna sheria za FIFA zilizovunjwa bali sheria zilizovunjwa ni za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,”
“Huko atapoteza muda na anaweza kuadhibiwa zaidi maana kwanza kabla ya kufungua kesi unatakiwa uweke kama dola Elfu 10 (Sh Milioni 23 za Tanzania) tena hiyo uwe na uhakika kama utashinda, ukishindwa adhabu yake inaweza kuwa kubwa kwake Fei, hivyo awe makini na wale wanaomshauri” amesema Rage
Kwa mujibu wa Baba Mlezi wa Feisal Salum ‘Fei Toto’ yupo Kisiwani Unguja ‘Zanzibar’ kwa mapumziko, akisubiri taratibu nyingine za kusaka haki yake baada ya Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF kumtaka arejee Young Africans.