Menaja wa Habari na Mawasilino wa Klabu ya Simba SC Ahmed Ally amefichua sehemu ya mazungumzo kati Rais wa Heshima na Mwekezaji Mwenza wa Simba SC Mohamed Dewji ‘Mo’, alipotinga Kambini huko Dubai juzi Jumanne (Januari 10).

Mo Dewji alizungumza na Wachezaji pamoja na Benchi la Ufundi la Simba SC linaloongozwa na Kocha kutoka nchini Brazil Roberto Oliveira Gonçalves do Carmo ‘Robertinho’.

Ahmed Ally amefichua sehemu ya Mazungumzo hayo kwa kunukuu kauli ya Mo Dewji, kwa kuandika katika kurasa zake za Mitandao ya Kijamii.

Sehemu ya nukuu ya Mo Dewji iliyotumiwa na Ahmed Ally katika andiko lake, imethibitisha mapenzi ya mwekezaji huyo na Klabu ya Simba SC, huku akisisitiza hajaondoka na hataondoka kwenye klabu hiyo ambayo amekuwa akikiri kuipenda tangu akiwa mtoto mdogo.

Ahmed Ally ameandika: “Juzi kwenye kikao cha Rais wa heshima @moodewji na kikosi aliwaambia wachezaji kuwa duniani yeye anapenda timu moja tuu Simba Sports ?

Akasema Simba ikifungwa maumivu ya kesho ni makali mnoo na ikishinda furaha yake haina mfano
Akasema mimi nimekuja Simba kwa sababu ya mapenzi na hakuna cha kunitoa Simba kwa sababu mapenzi hayaishi

Akawaambia wachezaji nyie chezeni mpira msisikilize kelele za watu eti Mo kaondoka, Niende wapi na hii ndo timu ninayoipenda nitafanya kila kitu kuhakikisha natimiza ndoto yangu ya kutwaa ubingwa wa Afrika siku moja”

Simba SC imeweka kambi Dubai-Falme za Kiarabu ikijiandaa na Mshike Mshike wa Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.

Ikiwa huko Simba SC itacheza michezo miwili ya kirafiki dhidi ya Dhafra FC ya UAE na CSKA Moscow ya Urusi.
Simba SC itaanza kucheza mchezo wake wa kwanza wa Kirafiki kesho Ijumaa (Januari 13) dhidi ya Dhafra FC majira ya saa kumi na moja jioni kwa saa za Tanzania, na Jumapili (Januari 15) itacheza dhidi ya CSKA Moscow iliyoweka kambi ya maandalizi Dubai.

Wanasayansi wagundua Sayari yenye ukubwa wa Dunia
Rage amshauri tena Feisal Salum