Mwenyekiti wa zamani wa klabu ya Simba Ismail Aden Rage amesema hana shaka na kikosi cha klabu hiyo, kuelekea mchezo wa mkondo wa kwanza wa hatua ya awali wa Ligi ya mabingwa Barani Afrika dhidi ya Plateau United.
Simba SC watacheza ugenini Jumapili (Novemba 29) mjini Jos- Nigeria huku mashabiki na wanachama wake wakiwa na matumaini makubwa kupata matokeo mazuri.
Rage amesema: “Sina matatizo na Simba katika michuano hii ya ligi ya mabingwa kwani tuna rekodi nzuri huko nyuma, sisi ndio timu ya kwanza kutwaa Kombe la CECAFA mwaka 1974, pia mwaka huo huo tulifanikiwa kuweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza kufika nusu fainali ya klabu Bingwa Afrika katika ukanda wetu, hivyo sina shida nayo.
“Lakini kocha anatakiwa kwenda kwa tahadhari kubwa kuelekea mchezo huo kwani tuna historia mbaya na timu za Nigeria kila tukipangiwa kwani tumekuwa hatuvuki mbele yao, hivyo wanahitaji kuwa na maandalizi ya kutosha kuelekea mchezo huo.
“Lakini kwa safari hii jinsi kikosi kilivyo nina imani tutafanikiwa kuvuka, kikosi kipo vizuri.”
Mpambano wa Plateau United na Simba SC utaunguruma kuanzia saa kumi jioni kwa saa za Nigeria sawa na saa kumi na mbili kwa saa za Afrika Mashariki, kwenye Uwanja wa New Jos wenye uwezo wa kuchukua watu 40,000, lakini kutokana na janga la Corona, mashabiki hawatoruhusiwa kuingia uwanjani hapo.