Kikosi cha mabingwa wa soka Tanzania Bara Wekundu Wa Msimbazi Simba leo Ijumaa, Novemba 27 kinafanya safari ya kuelekea mjini Jos yalipo makao makuu ya Plateau United, tayari kwa mchezo wa mkondo wa kwanza wa hatua ya awali wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.  

Mpambano huo utaunguruma Jumapili, Novemba 29 saa kumi jioni kwa saa za Nigeria sawa na saa kumi na mbili kwa saa za Afrika Mashariki, kwenye Uwanja wa New Jos wenye uwezo wa kuchukua watu 40,000, lakini kutokana na janga la Corona, mashabiki hawatoruhusiwa kuingia uwanjani hapo.

Simba SC ilifikia mjini Abuja tangu juzi Jumatano (Novemba 25) na umbali kutoka mjini humo hadi Jos, ni Kilomita 300 kwa usafiri wa basi, lakini kufuatia usalama wa nchi wa Nigeria kuwa shakani katika kipindi hiki, huenda mabingwa hao wa Tanzania Bara wakatumia usafiri wa ndege.

Simba imeshauriwa kutumia usafiri wa ndege kwa kuwa katikati ya miji hiyo kumekuwa na matukio ya utekaji watu ikiwa watatumia usafiri wa basi.

Balozi wa Tanzania nchini Nigeria, Dk Benson Bana amekuwa kati ya watu waliotilia mkazo suala hilo la kutumia usafiri wa ndege, alipozungumza na viongozi na wachezaji wa Simba alipowatembelea kambini jana Alhamis Novemba 26.

Balozi huyo amesema kuwa anaamini timu hiyo itafanya vizuri na kikubwa ambacho kinahitajika ni ushindi katika mchezo huo.

Wakati Simba wakifanya safari ya kutoka mjini Abuja kuelekea Jos, wawakilishi wengine wa Tanzania kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika Namungo FC, wamekamilisha maandalizi ya mchezo wa mkondo wa kwanza dhidi ya Al Rabita ya Sudan Kusini utakaochezwa kwesho uwanja wa Azam Complex Chamazi, Dar es salaam.

Namungo FC wanashiriki kwa mara ya kwanza michuano hiyo, baada ya kumaliza katika nafasi ya pili kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Tanzania (ASFC), kufuatia kufungwa na Simba SC kwenye mchezo wa fainali uliochezwa mwezi Agosti mjini Sumbawanga, mkoani Rukwa.

Mwanasheria Mkuu aionya CHADEMA, kamati kuu kuamua
Kenya yarejesha masharti kudhibiti Covid 19

Comments

comments