Aliyekua mwenyekiti wa klabu bingwa Tanzania bara Simba SC Ismail Aden Rage, amesisitiza kwamba klabu hiyo kongwe hapa nchini imeweka historia nyingi ambazo wapinzani wao young Africans hawawezi na hawata thubutu kuzivunja.
Rage amejitamba kwa kubeza young Africans kwa upande huo, ikiwa ni sehemu ya utani unaendelea kudumishwa baina ya viongozi, wanachama na mashabiki wa klabu hizo pendwa hapa nchini.
Rage amesema moja kati ya historia iliyowekwa na Simba ni kuweka kambi ya siku 45 nchini Brazil kujiandaa na ligi mwanzoni mwa miaka ya 80 huku Young Africans wakijitutumua lakini walikaa kambi ya siku 8 tu nchini humo.
Pia akaanika jambo lingine ambalo Simba inaendelea kujitambia kuwa ni kuendelea kuwa klabu pekee iliyokuwa na ubavu wa kumsajili mchezaji yeyote waliokuwa wanamuhitaji kutokana na msuli mkubwa wa kifedha waliokuwa nao kiasi cha kuzifanya klabu nyingine kuwa wanyonge linapokuja suala la usajili kwa wakati huo.
Amesema Simba ndiyo klabu iliyokuwa ikizifunga magoli mengi klabu nyingine ilizokuwa ikikutana nazo kwenye michuano ya ndani nan je ya nchi.
Historia nyingine ambayo Simba iliweka ni umafya wa kupora wachezaji kutoka kwa wapinzani wao Young Africans, ingawa mara chache walikumbana na wakati mgumu kutoka kwa makomandoo watiifu wa klabu pinzani, ikiwemo kushindwa kumsajili mchezaji Makumbi Juma ‘Homa Ya Jiji’ waliyejaribu kumpora kwa wakati huo.
Rage amekua sehemu ya wadau wa klabu za Simba na Young Africans wanaopenda kuendeleza utamaduni wa utani, lakini wakati mwingine hupongeza kwa mazuri ambayo yamekua yakifanywa na wapinzani wao.
Siku za karibuni mdau huyo ambaye aliwahi kuwa katibu mkuu wa chama cha soka nchini (FAT) kwa sasa Shirikisho la soka (TFF), alipongeza hatua ya katiba ya Young Africans kuwa na kipengele kinachotoa mwanya mzuri pindi watakapokua kwenye mchakato wa kuelekea kwenye mabadiliko.
Rage amesema kipengele hicho kinatoa nafasi kwa mchakato huo kupelekwa kwenye jumuia, tofauti na klabu nyingine ambapo baadhi ya watu hujifungia na kufanya maamuzi kabla kuwafikishia wanachama ili kufanya maamuzi.