Aliyekuwa Rais wa Mali Ibrahim Boubacar Keïta aliyetolewa madarakani kupitia mapinduzi ya kijeshi amelazwa katika hospitali moja mji mkuu, Bamako.
Kwa mujibu wa Shirika la habari la Associated Press lilinukuu vyanzo viwili katika kliniki ambayo kiongozi huyo wa zamani anaripotiwa kutibiwa.
Ibrahim Keïta (75) alizuiliwa kwa siku kumi na wanajeshi kabla ya kutangaza kujiuzulu na baaadae kuachiliwa huru.
Wakati wa mazungumzo yakifanyika kutafuta muafaka wa mzozo wa kisiasa nchini Mali Keita alinukuliwa akisema kuwa hana haja ya mamlaka ya urais.
Ikumbukwe miezi kadhaa upinzani ulikuwa ukimshinikiza rais huyo kujiuzulu na kumlaumu kwa kurudisha nyuma uchumi wa nchi, kushindwa kudhibiti ufisadi na kukabiliana na makundi ya kigaidi.