Makumi elfu ya waandamanaji nchini Togo wamejitokeza barabarani katika mji mkuu wa nchi hiyo, Lome kwa kile wanachodai kuwa ni hatua ya mwisho ya kampeni yao ya kumlazimisha Rais Faure Gnassigbe kuondoka madarakani.
Maelfu ya waandamanaji wengine walionekana katika jiji la Sokode ambalo ni jiji la pili kwa ukubwa nchini humo. Waandamanaji hao wamefunga njia zote muhimu katikati ya jiji zinazounganisha upande wa Kusini na Kaskazini mwa nchi hiyo.
Waratibu wa maandamano hayo wameliambia Shirika la Habari la AFP kuwa ‘hili ni onyo la mwisho’ kwa utawala wa Rais Gnassigbe na kwamba waandamanaji wamekumbwa na hasira kali.
Kiongozi wa kampeni hiyo, Jean-Pierre Fabre amesema kuwa wataendelea kuongeza nguvu ya maandamano hayo kuilazimisha Serikali kutii matakwa ya umma.
Lengo kuu la waandamanaji hao ni kutaka kurejeshwa kwa kipengele cha katiba ya nchi hiyo ya mwaka 1992, kipengele kinachoweka ukomo wa mihula miwili kwa Rais.
Hadi sasa, Rais Gnassigbe anatumikia muhula wa tatu tangu alipoingia madarakani mwaka 2005. Rais huyo alichukua nafasi ya urais iliyokuwa inashikiliwa na baba yake, hali inayopelekea familia yake kuwa imeiongoza Togo kwa miaka 50.
Katika maandamano hayo yaliyoanza kushika hatamu mapema mwezi uliopita, takribani watu wanne wameripotiwa kupoteza maisha na mamia kujeruhiwa.