Waziri Mkuu wa Sri Lanka, Ranil Wickremesinghe ambaye naye alitangaza kujiuzulu hii leo Julai 13, 2022 ameteuliwa kuwa Rais wa mpito wa nchi hiyo.
Spika wa Bunge la Sri Lanka, Mahinda Yapa Abeywardena amesema Waziri Mkuu ameteuliwa kuwa Kaimu Rais baada ya Rais wa nchi hiyo Gotabaya Rajapaksa kudaiwa kuikimbia nchi hiyo yeye na familia yake.
Hata hivyo Spika huyo amesema uteuzi wa Waziri Mkuu kukaimu nafasi hiyo umefanywa na Rais Gotabaya Rajapaksa kabla hajaondoka nchini humo.
“Alinifahamisha kuhusu uteuzi huo chini ya Kifungu cha 37.1 cha katiba ya nchi yetu ya Sri Lanka,” amesema Spika Mahinda Yapa.
Hatahivyo, hakuna neno la moja kwa moja lililotolewa na Rais Rajapaksa mwenyewe, ingawa matangazo yote ya nchi katika siku zote za hivi karibuni katika siku za hivi karibuni yametolewa na Spika wa Bunge na Ofisi ya Waziri Mkuu.
Kwa mujibu wa Katiba ya Sri Lanka, nafasi ya Rais ikiwa wazi, Waziri Mkuu ataapishwa na kukaimu kwa muda mpaka atakapochaguliwa Rais mwingine kutoka miongoni mwa wabunge.
Uchaguzi huo, unapaswa kufanyika ndani ya siku 30 baada ya Rais kujiuzulu, huku Spika Mahinda akisema uchaguzi unaweza kufanyika Julai 20, 2022.
Rais wa Sri Lanka Gotabaya Rajapaksa ameikimbia nchi hiyo kwa ndege ya kijeshi, huku kukiwa na maandamano makubwa kuhusu mzozo wa kiuchumi.
Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 73 amekimbilia Maldives.