Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali inaunga mkono jitihada za kuanzisha Kamati ya Kuzuia Udhalilishaji wa kijinsia Zanzibar pia ameziagiza taasisi zote zenye wajumbe wanaounda kamati hiyo kutoa ushirikiano na kufanya kazi kwa ukaribu na Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ili kufanikisha malengo yanayokusudiwa.
Dkt. Mwinyi ameyasema hayo hii leo Juni 1, 2023 wakati akizindua Kamati ya kuzuia Udhalilishaji wa kijinsia Zanzibar katika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdul-Wakil Kikwajuni, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Amesema, kamati hiyo inatakiwa kufanyia kazi ya kuchunguza athari za matumizi ya mitandao ya kijamii na ongezeko la kesi za udhalilishaji nchini pia amependekeza kuliangalia suala zima la matumizi na athari za mitandao ya kijamii kwa vijana endapo mitandao hiyo ikitumiwa vibaya inaweza kuwa kishawishi kimojawapo cha vitendo vya udhalilishaji.
Aidha, Dkt. Mwinyi amesema Serikali inafarijika kuona jamii inaguswa na uzito wa janga hili kwa kuzingatia madhara yake na kubuni mbinu mwafaka kuvikabili vitendo hivyo pamoja na kupiga vita janga la udhalilishaji wa Watoto na unyanyasaji wa kijinsia.