Kocha Msaidizi wa Polisi Tanzania, John Tamba, amesema maandalizi ya kikosi chao yapo vizuri kuelekea mechi ijayo ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Simba SC ambayo inatarajiwa kupigwa Juni 6, mwaka huu kwenye Dimba la Azam Complex ambapo wanahitaji matokeo mazuri.

Tamba amesema: “Tayari maandalizi yanaendelea kwa ajili ya mechi yetu, kikubwa tutapambana kwa ari na morali ili kuondoka na pointi tatu.

“Hali ya wachezaji kwa ujumla ipo vizuri, wana ari na morali kupambana na wanajua nini tunachokihitaji kwenye mchezo huo.

“Wapinzani wetu ni wazuri, tutaingia kwa tahadhari kubwa na kuwaheshimu ili kupata alama tatu kujinusuru kushuka daraja maana nafasi ambayo sio nzuri kwa upande wetu.

“Mashabiki wasikate tamaa wajitokeze kwa wingi kuja kuangalia burudani ya kutosha tuwahakikishie iwe jua iwe mvua ushindi tunahitaji kwa hali yoyote.”

Polisi Tanzania inashika nafasi ya 15 katika Ligi Kuu Bara baada ya kucheza mechi 28, ikiwa na pointi 25, inapambana kuepuka kushuka daraja ikibakiwa na mechi mbili.

Mkopo: Mbunge ataka Vijana wapewe semina
Rais Dkt. Mwinyi azindua kamati kuzuia udhalilishaji