Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli ameahidi kutoa Sh 400 Milioni kwa ajili ya kufanikisha ujenzi wa kituo cha afya katika eneo la Kisaki, Morogoro vijijini.
Mkuu huyo wa nchi alitoa ahadi hiyo alipokuwa akizungumza na wananchi wa eneo hilo akiwa anaelekea Rufiji kwa ajili ya kuweka jiwe la msingi la mradi wa Stigler’s Gorge utakaozalisha umeme wa megawati 2,115.
Aidha, Rais Magufuli aliwaagiza Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Suleiman Jafo kutumia siku saba kutafuta eneo la kujenga kituo hicho cha afya na kuanza mara moja ujenzi huo. Aliwataka mawaziri hao kuusimamia ujenzi huo kikamilifu.
“Kwanini hakuna kituo cha afya na kuna watu wengi hapa?” Alihoji. “Nataka kituo cha afya kianze kujengwa mara moja, nitamuagiza Waziri wa TAMISEMI ashughulikie,” aliongeza.
Alisema kuwa kituo hicho cha afya kitakuwa kimejengwa na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi-Tafa, ambaye ni yeye (Dkt. Magufuli).