Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli, amefanya uteuzi wa viongozi watatu kushika nafasi mbalimbali katika kampuni za simu za mkononi za Airtel na TTCL.
Katika uteuzi huo, amemtoa aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya TTCL Dkt. Omary Rashid Nundu ambaye amempeleka kuwa Mwenyekiti mpya wa Bodi ya Airtel Tanzania.
Nafasi ya Omary Nundu imechukuliwa na Mohammed Abdallah Mtonga ambaye uteuzi wake umeanza leo Juni 12, 2019. Mtonga alikuwa mkaguzi wa ndani wa Wizara ya Fedha.
Uteuzi wa Dkt. Omari Rashid Nundu katika nafasi hiyo unafuatia makubaliano yaliyofikiwa kati ya Serikali ya Tanzania na kampuni ya Bharti Airtel International juu ya uendeshaji wa kampuni ya simu za mkononi ya Airtel Tanzania ambapo Mwenyekiti wa Bodi ya Airtel Tanzania anapaswa kuteuliwa na Serikali ya Tanzania.
Kwa mujibu wa makubaliano hayo Afisa Mkuu wa Ufundi (Chief Technical Officer – CTO) pia anateuliwa na Serikali ya Tanzania, na aliyeteuliwa kushika nafasi hiyo ni Dkt. Prosper Godfrey Mafole.
Wajumbe wengine watakaoiwakilisha Serikali katika Bodi ya Airtel Tanzania ni John Marato Sausi pamoja na Lekinyi Ngariapusi Mollel.