Ombi la Mbunge wa Kigamboni, Dk Faustine Ndugulile la Serikali kuangalia upya tozo za Daraja la Kigamboni liligonga mwamba baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kusisitiza kuwa tozo hiyo inatokana na deni la gharama za ujenzi wa mradi huo.
Ndugulile, alitoa ombi hilo wakati akitoa salamu kwenye uzinduzi wa mradi wa maji Kigamboni, ugawaji vifaa vya uchimbaji visima na makabidhiano ya eneo la bwawa la Kidunda kwa mkandarasi, ambapo akatumia nafasi hiyo kumuomba Rais Samia kuangalia utaratibu wa kuondoa tozo hiyo.
Alisema, “Kigamboni unaingia kwa hela kila siku na lazima urudi kwa hela, kwa hiyo hili nalo Mheshimiwa Rais kama nalo unaweza kwenda kuliangalia nitashukuru sana,” huku Rais akimjibu kuwa, “uwezekano uliopo ni kupunguza tozo hiyo, lakini si kuiondoa kabisa.”
Rais Samia alisema, “Ni kweli Daraja la Kigamboni tunatoa tozo lakini hii imetokana na mradi wenyewe ulivyojengwa. Daraja la Kigamboni ni mkopo na kama ni mkopo lazima tuurudishe na hakuna wa kurudisha zaidi ya sisi wenyewe wananchi ni uzoefu wa kwanza kuona wananchi wanalipa kupita pale.”