Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amemkabidhi nyumba ya kuishi Rais mstaafu, Jakaya Kikwete iliyojengwa Wilaya ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam.
Nyumba hiyo imejengwa na Serikali ya Tanzania kupitia Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) ikiwa ni utekelezaji wa kifungu namba 12 cha sheria ya mafao ya hitimisho la kazi kwa viongozi wa siasa sura ya 225 na marejeo ya mwaka 2020.
Kifungu hicho kinaelekeza kuwa pamoja na stahili nyingine za matunzo ya viongozi wakuu wastaafu, rais mstaafu anastahili kujengewa nyumba ya kuishi yenye hadhi ya rais.
Akizungumza baada ya kukabidhi nyumba hiyo leo Jumapili Mei 9, 2021, Rais Samia amemhakikishia Kikwete kuwa Serikali itaendelea kumtunza yeye na viongozi wengine wastaafu kama inavyoelekezwa katika sheria.
Amebainisha kuwa Serikali itafanyia kazi uboreshaji wa sheria hiyo pamoja na kuhakikisha wajane, wagane wa viongozi wanatunzwa.
Rais Samia ametumia fursa hiyo kumuagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora. Mohamed Mchengerwa kuanza maandalizi ya kutimiza haki zote anazostahili aliyekuwa rais wa awamu ya tano, Hayati John Magufuli.