Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), limesema limepokea kwa mshituko na masikitiko kauli ya
Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO), na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa kuwa Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Huduma za Habari (MSA 2016), umeshindwa kuingizwa bungeni kutokana na ripoti nyingi za Kamati za Kisekta za Bunge.
TEF kupitia taarifa yake imeeleza kuwa, sababu iliyotolewa ni nyepesi na inapata wasiwasi iwapo kuna utashi wa kufanya mabadiliko katika sheria hii. Katika vikao vilivyotangulia, tumeuona ugumu kutoka kwa baadhi ya maofisa wastaafu walioazimwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), maafisa kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, na baadhi ya vyombo vya ulinzi na usalama wakionesha wazi kutokuwa na nia ya kurekebisha sheria hiyo.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa, vikao walivyofanya, viliisha bila mwafaka katika vifungu mbalimbali ikiwamo Mamlaka ya Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) chini ya vifungu vya 9 na 10, ambavyo vinampa mamlaka ya kuwa mlalamikaji, mwendesha mashitaka, mtoa hukumu na msimamizi wa utekelezaji wa hukumu; suala tunalosema ni ukiukwaji wa Utawala Bora na Utawala wa Sheria.
Aidha, imeeleza kuwa taaluma nyingine nchini, mabaraza yake au bodi zake ndizo zinazofanya kazi hii, ila maafisa hawa wachache, wanang’ang’ania sekta ya habari madaraka haya yawe katika mikono ya mtu mmoja, Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO), suala ambalo hawakubaliani nalo.
“Ilituchukua hadi kikao cha Novemba 21, 2022 Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya
Habari, Nape Nnauye alipolazimika kusimamia kikao hicho ndipo maafisa hao watatu wakakubali
kwa shingo upande kusema watarekebisha vifungu hivyo ili viendane na viwango vya kimataifa.
Kinachotushangaza, baadhi ya vifungu wanavyoving’ang’ania kama kashfa kugezwa jinai, tayari
vimefutwa kwenye sheria mama ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16.” imeeleza taarifa hiyo.
Taarifa hiyo imefafanua kuwa, “Tumekuwa na mawasiliano mazuri na Waziri Nape; Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Dkt. Eliezer Feleshi; Mwandishi Mkuu wa Sheria wa Serikali, Onorius Njole; na Ofisi ya Bunge, ila maafisa wachache wa chini ndiyo kwa muda mrefu wamekwamisha mabadiliko ya sheria hii.”
Aidha, TEF imesema “kwa namna ya ajabu, muswada huu umeshindikana kuingia bungeni tena (Februari, 2023). Tunajiuliza kama taarifa za kamati zimezuia muswada kuingia bungeni, je, muswada huu utapataje nafasi kwenye mkutano ujao wa Aprili, 2023? Je, itawezekana
vipi katikati ya hotuba za Bunge la Bajeti la mwaka 2023/2024?”
Suala la kubadili sheria hii limekaa muda mrefu. Sisi tunapodai Uhuru wa Habari si kwa sababu
ya wanahabari pekee, hapana. Uhuru huu ni wa Watanzania wote kutoa maoni yao; na kwa kufanya
hivyo tunakuza demokrasia nchini na kuongeza uwajibikaji.
Juni 28, 2021, Rais Samia Suluhu Hassan alielekeza TEF na wadau kukaa na Wizara
inayosimamia habari kuzungumza jinsi ya kubadili sheria hiyo ili ikidhi viwango vya kimataifa na
kwamba wakikwama wasisite kurudi kwake.
“Basi tunaomba Rais Samia atupe nafasi ya kukutana naye tumweleze wapi tumekwama na
wanaokwamisha ni kina nani, pengine akiwauliza yeye watampa majibu ya msingi kuliko
tunavyoshuhudia wakitupuuza sisi kwenye vikao,” imeeleza semehu ya taarifa hiyo.
Jukwaa la Wahariri na Wadau, kwa kuona kazi kubwa anayoifanya Rais Samia ya kurejesha uhuru
katika sehemu mbalimbali nchini ikiwamo kufungulia magazeti ya Mwanahalisi, Mseto, Tanzania
Daima na Mawio, kurejesha Bunge Live, kushusha bei za leseni za TV na Radio, TEF inaamini kuwa njia ya diplomasia ingewafikisha katika nchi ya ahadi, ila baadhi ya maafisa hawako tayari
kuona uhuru wa habari ukirejea nchini.