Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, leo Julai 15, 2021 amepokea mualiko wa kuhudhuria maonesho ya biashara ya kimataifa Dubai (Dubai Expo) yanayotarajiwa kufanyika mwezi Machi, 2022.
Amepokea mwaliko huo Ikulu Jijini Dar es Salaam baada ya kukutana na Mjumbe Maalum wa Mfalme wa Umoja wa Falme za Kiarabu (U.A.E) Sheikh Shakhboot Bin Nahyan Al Nahyan na kufanya nae mazungumzo hususani katika ushirikiano.
Kwa upande wake Rais Samia ameshukuru Umoja wa Falme za Kiarabu (U.A.E) kwa kuendeleza ushirikiano na Tanzania na kumuahidi Mjumbe huyo Maalum kuwa Serikali itaendeleza mahusiano mazuri kwa ajili ya manufaa ya nchi zote mbili.
Aidha, Rais Samia amesema kumekuwa na ongezeko la usawa wa kibiashara kati ya nchi hizi mbili mwaka hadi mwaka na kuongeza kuwa Tanzania inaendelea kufanya maboresho ya kibiashara ili kuvutia zaidi wawekezaji.
Hata hivyo Sheikh Al Nahyan amemshukuru Rais Samia kwa kuendeleza ushirikiano na Nchi za Falme za Kiarabu na kumkabidhi barua yenye ujumbe maalum kutoka kwa Mfalme wa U.A.E Sheikh Mohamed Bin Zayed.
Amesema U.A.E itaendeleza ushirikiano na uhusiano na Tanzania katika nyanja mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuunga mkono usawa wa kijinsia na haki za wanawake hasa wakizingatia kuwa Rais Samia ni mfano bora kwa wanawake nchini Tanzania na dunia kwa ujumla.
Halikadhalika Sheikh Nahyan amesema U.A.E inaunga mkono jitihada za Rais Samia za kupambana na ugonjwa wa UVIKO 19 ambapo amesema Umoja wa Falme za Kiarabu upo tayari kuipatia Tanzania chanjo ya ugonjwa huo.