Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema uamuzi wake wa kuitenga wizara itakayoshughulikia jinsia, maendeleo, wanawake na wizara ya afya ni kuimarisha utekelezaji wa mipango na sera.
Amesema hayo leo Desemba 16, 2021 katika uzinduzi wa kamati ya ushauri ya kitaifa kuhusu utekelezaji wa ahadi za nchi kwenye jukwaa la kizazi chenye usawa katika ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete Dodoma.
“Sasa ndugu zangu unaweza kuona kwamba pamoja na jitihada zote tulizozifanya na mipangano na sera zote tulizoweka bado hatujafika tulipotakiwa kufika.”amesema Rais Samia
“Sasa ili tuweze kufika tunapotakiwa kufika lazima kuwe na usimamizi, uratibu, kutathimini na ufuatiliaji wa sera na utekelezaji wetu wa mipango. Wizara hizi mbili mkizitizama ni afya na…, uamuzi wangu ni kuitenga wizara itakayoshughulikia jinsia maendeleo wanawake na mambo mengine,” amesema.
“kutoka kwenye kuchanganywa na wizara ya afya kwa sababu tukiweka wizara ya afya na mambo mengine na hali tuliyonayo sasa duniani sekta ya afya pekee yake inachukua sura kubwa ya wizara hii kuliko vipengele vingine vilivyobaki.”
“Lakini kama tutatenga vipengelee vingine vilivyobaki na afya tukaisimamisha pekee yake usimamisizi wa sera, sheria na mambo mengine unaweza ukaenda vizuri na ukapata msukumo unaohitajika. Kwa hiyo hayo ndio maamuzi yangu na nitajaribu kumshawishi Rais wa Zanzibar naye afanye hivyo hivyo ili twende vizuri.”