Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia amemuomba mwenzake wa ZFF, Suleiman Mahmoud Jabir kuweka kanuni za kuwalinda wadhamini waliojitokeza kusaidia mpira wa Zanzibar.
Ombi hilo alilitoa hivi karibuni wakati akizungumza kwenye hafla maalumu ya uzinduzi wa Kamati ya Hamasa iliyoteuliwa na Shirikisho la Soka Zanzibar.
Alisema kwa muda mrefu ligi ya Zanzibar ilikuwa haina udhamini ambapo sasa wamejitokeza Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) kuidhamini ni lazima walindwe.
“Muwalinde PBZ, kwani wameingia kwenye Ligi ya Zanzibar hakuna mtu yeyote aliyekuwa anaitaka, lakini baada ya muda kuna benki zitajitokeza na kutaka kupiga picha na wachezaji, zitaingia mikataba, msiruhusu hilo,” alisema Karia.
Aidha, aliishukuru PBZ kwa kuiwezesha Ligi ya Zanzibar kuwa na heshima na baada ya benki hiyo kuanza na wengine watajitokeza kutaka kudhamini.
Alisema kuwa hata Bara watu walikuwa hawataki kudhamini lakini sasa kila mtu anataka kuingia.