Maafisa Jijini New York nchini Marekani wamesema kuwa wamelazimika kuchunguza madai ya kwamba Rais Donald Trump alisaidia familia yake kukwepa kulipa kodi ya mamilioni ya dola katika miaka ya 1990.
Kwa mujibu wa ripoti iliyochapishwa na gazeti la New York Times imemshutumu Rais Trump kwa kuhusika na mpango wa ulipaji kodi ubabaishaji pamoja na udanganyifu ili kuficha makadirio yanayomhusu yeye pamoja na ndugu na wazazi wake.
Msemaji wa Ikulu ya Marekani, Sara Sanders amesema kuwa malipo yote yalikuwa yakikaguliwa na kupitishwa na mamlaka za kodi kwa miaka mingi iliyopita.
Rais Trump bado hajasema lolote kuhusu madai hayo lakini mwanasheria wake, Charles Harder amekanusha vikali mteja wake kutenda kosa lolote.
Aidha, amesema kuwa hakuna udanganyifu au ukwepaji wa kodi uliofanywa na yeyote na kusema kuwa taarifa ambazo gazeti la New York limeegemea ni za madai ya uongo na yasiyo sahihi.
Hata hivyo, Gazeti hilo la New York Times katika taarifa yake limesema pamoja na kwamba Rais Trump amekuwa akijinadi kuwa ubilionea wake unatokana na jitihada zake binafsi, lakini amekuwa akipokea mamilioni ya dola kutoka rasilimali za wazazi wake tangu akiwa na umri wa miaka mitatu.